Monday, October 21, 2013

ASKARI WA HIFADHI WAUA MBELE YA KITUO CHA POLISI





 
NA DANIEL LIMBE
Askari wa Hifadhi ya Kisiwa cha Rubondo wilayani 
Geita mkoani hapa, wamekumbwa na kashfa nyingine
 baada ya kudaiwa kumuua raia mmoja kwa kipigo 
mbele ya kituo kidogo cha polisi Chato.
Aliyeuawa ametambulika kuwa ni Moshi Nkola
 (39), mkazi wa kijiji cha Mkuyuni kata ya
 Chato wilayani hapa.


Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Geita, Pudensiana Protas,
 alidai kutokuwa na taarifa ya tukio hilo na kuahidi kufuatilia
 ukweli wa jambo hilo kutoka kwa wasaidizi wake.
Akielezea tukio hilo, kaka wa marehemu, Paulo Nkola (42),
 aliliambia NIPASHE Jumapili kuwa nduguye alipigwa na 
askari wawili wa hifadhi ya kisiw
a cha Rubondo (hakuwataja majina) Oktoba 17, majira 
ya saa 4 usiku wakati akitoka kwenye duka la kuuza pombe.

Alisema kabla ya kipigo hicho, Nkola alikuwa akiendesha 
pikipiki yake wakati akirejea nyumbani kwake na baadaye
 alikutana na askari hao wakamtaka awabebe kwenye pikipiki
hiyo kwa nguvu kwa lengo la kuwapeleka kwenye mwalo wa
 kasenda ambapo kuna ghati la kuvukia ili kuingia ndani ya
 hifadhi hiyo.
Baada ya kukaidi amri ya askari hao, mmoja wao alipanda
 kwa makusudi wakati Nkola akitaka kuondoka eneo hilo, 
hali iliyosababisha kuyumba na kuanguka. Kitendo hicho 
kilichowaudhi askari hao na kuanza kumshambulia kwa kipigo.
Paulo alisema baada ya mdogo wake kuzidiwa nguvu, alilazimika
 kukimbilia kituo kidogo cha polisi cha Muganza ili kunusuru
 maisha yake, lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida watu hao 
walimfuata mpaka kituoni hapo na kuendelea kumpiga mbele ya 
askari wa polisi waliokuwa zamu.
Kutokana na kipigo hicho, Nkola alijeruhiwa vibaya na baadaye
 kuomba PF3 kwa ajili ya matibabu kwenye zahanati ya 
Nyabugera iliyopo kata ya Muganza.
Hata hivyo, baada ya hali ya Nkola kuonekana kuzidi kuwa 
mbaya, alilazimika kwenda hospitali ya wilaya ya Chato ili
 kupata huduma zaidi kabla ya kukumbwa na mauti hayo
 usiku wa kuamkia jana.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Mashaka Majige, maarufu
 kwa jina la Kishimba, alisema askari hao pia walikuwa wamelewa
 pombe ambapo walimtaka Moshi awabebe kwenye pikipiki kwa
 nguvu ambapo alikaidi amri hiyo.
Alisema hata baada ya merehemu kukimbilia kituo cha polisi na
 kuingia ndani, askari hao walimfuata na kumshambulia mbele
 ya askari waliokuwepo bila kuwazuia.
Diwani wa kata ya Muganza, Marco Maduka, amekiri kutokea 
tukio hilo na kudai kuwa askari hao walikuwa wametoka kwenye 
hifadhi ya kisiwa cha Rubondo na kwamba walionekana wakinywa
 pombe kabla ya kufanya ukatili huo.
Alidai kuwa askari hao ambao majina yao hayajafahamika mara 
moja, walimpiga mtu huyo ndani ya kituo cha polisi kabla ya
kukumbwa na mauti.
Jeshi la polisi wilayani hapa limekiri kuwapo kwa madai hayo 
na uchunguzi unafanyika. Hakuna aliyekamatwa kuhusiana na
 mauaji hayo.
NIPASHE Jumapili lilipomtafuta Ofisa doria mkuu wa hifadhi ya
 kisiwa cha Rubondo, aliyefahamika kwa jina moja la Chuwa ili
 kuzungumzia tuhuma hizo simu yake haikupatikana.
Mganga mkuu wa hospitali ya Wilaya ya Chato, Dk. Pius Buchukundi,
 alikiri kupokelewa kwa Nkola akiwa mgonjwa lakini wakati akipatiwa
 matibabu alipoteza maisha.
Uchunguzi wa kitabibu umebaini kuwa Nkola aliumia kichwa
 kutokana na kitu kisichojulikana kumgonga na kusababisha kupasuka
 baadhi ya mishipa iliyosababisha damu nyingi kuvuja eneo la jicho.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment